Sunday, January 9, 2011

VIDEO - Wananchi Wanapochoshwa na Maisha Magumu


Hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei ulipelekea wananchi nchini Tunisia kuamua kuandamana kuung'oa utawala wa miaka 27 wa rais wa nchi hiyo, hali hiyo sasa imehamia nchini Misri ambapo wananchi waliochoshwa na utawala wa miaka 30 wa rais Hosni Mubarak.
Wananchi wa Misri nao wameamua kuwaiga wananchi wa Tunisia kwa kuandamana nchi nzima kuung'oa utawala wa miaka 30 wa rais Hosni Mubarak.

Nchini Tunisia wananchi waliochoshwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ukosefu wa ajira, rushwa na mfumuko wa bei waliamua kuandamana baada ya mchuuzi mmoja wa mboga mboga wa nchini humo kuamua kujiua kwa kujichoma moto kupinga rushwa katika serikali ya Tunisia.

Hali kama hiyo inatokea hivi sasa nchini Misri ambapo wiki iliyopita watu kadhaa nchini humo walijichoma moto wakiiga kitendo cha mchuuzi huyo wa mboga mboga wa Tunisia.

Kesi ya kijana Khaled Said anayesemekana kuuliwa na polisi wa Misri mwaka jana nayo imechochea watu wengi kuingia mitaani wakitaka utawala wa miaka 30 wa Hosni Mubarak ufikie kikomo.

"Tumechoshwa sasa, hii sasa inatosha", alisema Sayid Abdelfatah, mwenye umri wa miaka 38 ambaye aliandamana mitaani akiwa amebeba bendera ya Misri.

"Mapinduzi ya Tunisia yamenipa hamasa ya kuungana na watu kuipinga serikali, kwakweli sikufikiria kama watu wengi kiasi hicho ", alisema.

Karibia nusu ya watu milioni 80 wa nchini Misri wanaishi chini ya mstari wa umaskini wakiishi kwa kipato kisichofika hata dola mbili kwa siku.

Kiwango kibaya cha elimu, huduma duni za afya na idadi kubwa ya watu wasio na ajira ndio chanzo kilichopelekea asilimia kubwa ya watu kukosa mahitaji muhimu.

Polisi wa Misri ambao wamekuwa wakidaiwa kuogopeka kwa kutumia nguvu zaidi panapozuka ghasia, wamekuwa wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Watu watatu wameishafariki hadi sasa kutokana na ghasia hizo zinazoendelea nchini Misri.

Chini ni VIDEO ya maandamano yanayoendelea nchini Misri.



VIDEO - Wananchi Wanapochoshwa na Maisha Magumu

No comments:

Post a Comment